“Mwaka 2016 tulikuwa kwenye msiba wa jirani yetu ambaye alifiwa na mama yake. Siku hiyo watu walikuwa wanalia sana na kusikitika kwa kifo kile kilichotokea. Kitu kimoja ambacho kilimshangaza kila mtu ni kwamba mtoto wa kiume wa marehemu alikuwa hana machozi na wala hana huzuni sana kama ambavyo wengi walidhani itakuwa hivyo.

Watu wakajikuta wanajiuliza sasa mbona huyu hana hata huzuni na wala halii kama wengine? Mtu mmoja akajitoa mhanga akamfata na kumuuliza mbona wewe ndugu huoneshi kama una huzuni kubwa sana yaani upo kawaida tu? Yule mtoto wa marehemu akajibu na kusema hata kama nitalia machozi na kujigaragaza chini kuliko wote hapa hakuna kitakachobadilika. Tena ninaweza kusababisha matatizo mengine makubwa Zaidi. Cha muhimu ni kwamba hali hii imeshatokea tuwe wavumilivu tuweze kulimaliza hili lipite.

Usiku wake nikaamua kumfata na kumuuliza swali, hivi kaka umewezaji kukaa bila huzuni? Ukizingatia huyu ni mama yako? Akanieleza kwamba mama yangu alipokuwa mzima alikuwa anaumwa na kuteseka sana, niliumia sana kumuona akiwa anateseka, japokuwa sikuwahi kulia lakini nilikuwa na maumivu makali sana ndani yako. Kinachonipa faraja kwa sasa ni kuwa amepumzika na hateseki tena kama alivyokuwa hai.

Ndugu huyu akanieleza kwamba mama yake alikuwa anaugua kansa japokuwa wengi walikuwa hawafahamu. Akanieleza pia furaha na huzuni zipo katika uwezo wa mtu. Ni vile ambavyo wewe unachagua kipi kiwe kukubwa ndani yako.”

Ukweli ni kwamba maumivu yeyote unayopitia ndani ya moyo wako ni wewe mwenyewe umeamua.

Furaha ambayo unayo sasa ni wewe binafsi umeamua, japokuw ainawezekana kuna jambo limetokea bado wewe ndio mwenye maamuzi ya kufurahia au kuendelea kuona kile ulichokipata hakijatosha.

Rafiki yangu usikubali jambo ambalo lipo kwenye uwezo wako wa kufanya maamuzi likakuumiza moyo wako.

Yapo mengi yanatokea na ni nje ya uwezo wako lakini bado kuna yale ambayo yanakuwa upande wako wewe kuamua.

Kuna msemo unasema “Tatizo sio Tatizo bali ule mwitikio wako kwenye tatizo ndio tatizo” yaani mtazamo wako kwenye kile kinachoendelea maishani mwako ndio unaamua kiwe tatizo au fursa.

Mnaweza kuishi watu wawili kwenye mtaa wenye tatizo la maji halafu wote mna pesa. Mmoja kwasababu ana pesa akaamua kuhamia sehemu ambayo haina tatizo la maji na yule mwingine kwasababu ana pesa akaamua kuchimba maji chini na kuwauzia watu wa eneo lile maji na yeye akaendelea kupata maji ya kutosha.

Kuna mengi yanatokea kwenye Maisha yetu kila siku, wewe unaweza kuchagua kuumia na kulalamika, mwenzako anaweza kuchagua upande mzuri na akanufaika.

Hakikisha kile ambacho umekichagua kinakunufaisha wewe na wengine kwenye hali yeyote unayopitia.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

4 Responses

      1. Nimefurahishwa sana na ujumbe huu. Mungu akubariki sana na azidi kukupa mafunuo ya kuandika zaidi na zaidi mambo yenye mguso namna hii.

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading